Polisi wamepambana tena kwa ghasia na waandamanaji wanaopinga serikali ya Uturuki
Mapambano yaliyoanza Ijumaa yanaendelea kusambaa.Kitovu cha maandamano ni medani ya Taksim mjini
Istanbul ambako polisi wametumia moshi wa kutoza machozi na ambapo
ghasia nyingi zilitokea Ijumaa. Mkaazi mmoja wa Istanbul aliiambia BBC kwamba watu zaidi wanaelekea katika eneo hilo: "Watu 40,000 wanavuka daraja ya Bosphorus kutoka
upande wa Uturuki ulioko Asia kuja ng'ambo ya Ulaya kujiunga na
maandamano katika medani ya Taksim. Safari zote za treni zimesimamishwa ili kuzuwia
watu wasije, lakini wanatembea kwa miguu - kila mtu anatembea - na hapa
nilipo naweza kusikia ghasia kutoka medani ya Taksim. Tuko kama mwendo wa dakika 5 tu kutoka medani. Kwa hivo nafikiri maandamano yanaendelea na pengine kuwa ya ghasia zaidi kushinda Ijumaa." Maandamano yalianza siku nne zilizopita kupinga mpango wa kujenga maduka katika bustani iliyo karibu na medani ya Taksim. Waandamanaji, ambao wengi ni vijana, wanaishutumu serikali ya chama cha Kiislamu kwamba inakuwa ya kimabavu.

Chapisha Maoni