Madaktari wamesema uvaaji wa suruali za kubana kwa wanaume ni chanzo cha baadhi kuwa wagumba na wengine kupata magonjwa ya ngozi
Hata hivyo, watu wengi wanamfahamu kwa mitindo ya uvaaji wake wa suruali za kubana.
“Mitindo ni kama umri, haiwezi kuwa vilevile. Ni
kama vile mvinyo mtamu, pamoja na umri, mtindo wako lazima uwe na
mwonekano mzuri. Ni kujaribu kitu kipya. Mimi ni mtu mwenye kuthubutu na
napenda kujaribu vitu vipya (ikiwamo mitindo) ili kufanya maisha yangu
yawe yenye mvuto,” alisema Denzel.
Pamoja na tabia yake ya kupenda kuvaa suruali za
kubana kuna watu akiwamo dada yake hakupendezwa na hali hiyo, siku moja
dada yake alimwambia hapendezwi na uvaaji huo.
“Miaka miwili iliyopita, dada yangu aliniambia
kuwa uvaaji wangu wa suruali za kubana unaweza kuwafanya watu wanihisi
mimi ni ‘shoga’. Lakini nilimueleza uvaaji huo ni mtindo wa maisha
yangu,” alisema Denzel aliponukuliwa na gazeti la New Vision la Uganda.
Ingawa dada yake anauona uvaaji wake unalingana na
wanaume wenye vitendo vya ushoga, aliendelea kutetea kuwa mpenzi wake
wa kike amekuwa akimsifia kwa uvaaji wake wa suruali za mtindo wa
kubana.
Hata hivyo, siyo watu wa kawaida pekee ndiyo wenye
kukwazwa na mtindo wa uvaaji wa nguo za kubana wa Denzel. Hata
madaktari nao wametoa ushauri wao kuwa uvaaji wa suruali za kubana ni
hatari kiafya.
Lakini hoja za madaktari hazionyeshi kumteteresha
Denzel ambaye alijibu kwa kusema kuwa ni madaktari hao hao wanaosema
kunywa maji kwa kutumia vyombo vya planstiki ni hatari. Je? tumeacha
kunywa maji kwenye chupa za plastiki? Kila tunachofanya ni hatari. Kitu
kizuri ni kwamba sijawahi kuugua kwa sababu ya uvaaji wa mtindo wangu wa
suruali za kubana.”
Historia ya suruali za kubana
Mchambuzi wa masuala ya mitindo, Keturah Kamugasa
alisema suruali za kubana ni mtindo wa zamani ambao umerudi kwa kasi,
hasa kupitia suruali aina ya jinsi. “Zamani zilikuwa zikiitwa ‘bomba’.”
Suruali za kubana mwanzoni zilivaliwa na wanasiasa
wa kundi la mlengo wa kushoto la Sans-culottes, ambao walikuwa
wapinzani wakubwa wakati wa Mapinduzi ya Ufaransa, wakati huo suruali
hizo waliziita ‘pantaloons’.
Uvaaji huo ulianza kama uasi na kuwa mtindo wenye
umaarufu katika miaka ya 1950. Suruali hizo baadaye zikaanza kuvaliwa na
mastaa wa rock’n’roll katika miaka ya 1960 na kuendelea kusambaa katika
jamii.
Baadaye, mtindo huo ulishika kasi na suruali za kubana, mkunjo
mwembamba wa koti kifuani na tai nyembamba ukawa mtindo wa mavazi ya
jamii nyingi katika kipindi hicho.
Katika miaka ya 1970, vijana wa kiume walionekana
kuvaa suruali za kubana kuanzia kiunoni na mapajani, lakini chini
zinakuwa pana. Kuanzia hapo mtindo wa suruali za bugaluu au suruali
pana, ukazaliwa. Katika miaka ya 1980 mtindo wa rangi za kumeremeta kwa
wanaume ukaibuka.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mlimbwende wa Uganda, Miss
Uganda, Brenda Nanyonjo alieleza kuwa katika miaka 2000, enzi za kuweka
rangi za kumeremeta, mkunjo wa koti kifuani na suruali za kubana kwa
wanaume uliibuliwa upya na wabunifu wa mintindo wa kimataifa.
Mtindo wa wanaume wa kuweka rangi za kumeremeta kwa wanaume ukashika kasi katika ubunifu wa mitindo ya kileo kwa wanaume.
Matatizo ya kiafya
Dk Vincent Kafuuza wa Kituo cha Friends Polyclinic
& Ambulance Service alisema siyo tu kuhusu suruali za kubana,
lakini nguo zozote za kubana siyo nzuri kuwa mavazi ya kila siku.
Alieleza kuwa mwili unahitaji kupumua, hali ambayo
hufanyika kupitia kutoka jasho kwenye vinyweleo kwenye ngozi na jasho
linatakiwa kukauka lenyewe taratibu.
Dk Kafuuza alisema ikiwa mtu amevaa jinzi ya
kubana au nguo ya ndani ya kubana, jasho litagandana kwenye vinyweleo
vya ngozi na wakati mwingine inaweza kusababisha magonjwa ya ngozi kama
vile ‘fangasi’, maumivu ya mwili na vipele katika mapaja na sehemu
zingine za siri.
“Wanaume ambao wanavaa suruali za kubana wana hatari ya kupunguza kiwango cha mbegu za uzazi.
Na wakati mwingine zinaweza kupungua kwa kiwango
kikubwa na kumfanya mwanamume ashindwe kumpa ujauzito mwanamke,” alisema
Dk Kafuuza.
Dk Kafuuza alisema suruali za kubana zina kawaida
ya kusukuma ndani sehemu zinazotunza mbegu za uzazi za mwanamume, hali
inayosababisha matatizo kama vile uvimbe na ngozi kubabuka.
Nguo za ndani za kubana zinazuia kukuwa kwa mbegu za uzazi.
Wakati joto la kawaida la mwili ni sentigredi 37, mfuko wa mbegu
za uzazi wa mwanamume unahitaji kiwango cha joto kati ya sentigredi
35.5 na 36 ili kufanya kazi katika hali ya kawaida.
Dk Charles Kiggundu ambaye ni Mshauri wa Hospitali
ya Mulago na Chuo Kikuu cha Afya cha Makerere, alisema joto la mbegu za
uzazi za mwanamume linaweza kuongezeka ikiwa mfuko unaozishika utafifia
ndani ya mwili kwa muda mrefu, kwa mfano kama mwanamume amevaa nguo ya
ndani ya kubana.
Kwa mujibu wa Dk Lawrence Kazibwe wa Hospitali ya
Mulago, alisema mbegu za uzazi za mwanamume ziko kwenye mfuko maalumu
kwa sababu zinahitaji kuwa zimepoa zaidi ya maeneo mengine ya mwili, ili
ziwe kwenye mazingira tulivu.
Alisema lengo hilo linaweza kuvurugika iwapo
mwanamume atavaa suruali ya kubana ambayo itazifanya mbegu za uzazi
zikose mawasiliano ya kawaida na sehemu nyingine ya mwili, ambayo ni
kupata joto linalotakiwa.
“Baadhi ya wanaume wanafikiri kusafirisha mbegu za
uzazi pekee kwa mwanamke ndiko kunawezesha mwanamke kupata ujauzito,
lakini urutubishaji hauwezi kutokea katika sehemu za kikeni,
kwa kuwa mbegu za uzazi lazima zipite kwenye mrija unaotakiwa kukutana na mayai mengine.
Hivyo basi mbegu za uzazi zinahitaji kuwa na nguvu
na nyingi ili ziweze kuyafikia mayai ya kikeni na kuwezesha kupata
ujauzito,” alifafanua Kiggundu.
Kiggundu alisema; “Hebu fikiria katika hali ambayo
mbegu za uzazi ni chache na dhaifu! Hii ina maana hazitaweza
kurutubisha mayai ya kike.
Hivyo unaweza kutoa mbegu za uzazi wakati wa tendo la ndoa, lakini hakuna ubebaji mimba utakaofanyika.”
Mbegu za uzazi ambazo ni dhaifu, kama vile zile
ambazo hazina mkia, zenye mkia mkubwa, zenye mkia mdogo, zilizopinda
kichwani na zile zenye mikia miwili, haziwezi kupenye kwenye mrija wa
kwenda kwenye mayai ya uzazi ya kike.
Imeandikwa na Noor Shija kwa msaada wa mtandao.


Chapisha Maoni