Ptofesa Ibrahim Haruna Lipumba akizungumza na wafuasi wake
BARAZA Kuu la Uongozi la Chama cha Wananchi (CUF), limetangaza
kumfukuza uanachama Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Profesa Ibrahim
Lipumba. Amefukuzwa kwa kile kilichoelezwa kuwa amekwenda kinyume na katiba ya chama na kufanya uasi kwa wanachama.
Akisoma uamuzi huo jana mbele ya waandishi wa habari katika ofisi ya
chama hicho iliyopo Vuga mjini Zanzibar, Mjumbe wa Baraza hilo, Katani
Ahmed Katani, alisema Baraza Kuu hilo limechukua uamuzi huo chini ya
Kifungu cha Katiba Ibara ya 10 (1) (c) ambapo wajumbe wote wapatao 43
walipiga kura na kukubaliana na uamuzi huo.
Katani alisema baraza hilo limemtia hatiani Profesa Lipumba kwa
kitendo chake cha Septemba 24 mwaka huu, kuvamia ofisi ya chama akiwa na
kikundi cha watu waliowaita wahuni na kuwapiga walinzi huku
akisababisha uharibifu mkubwa wa mali za chama.
Aidha alisema baraza hilo limesikitishwa na vitendo vya dharau vya
Profesa Lipumba kwa kuwa katika barua ya tarehe 24 Septemba mwaka huu,
alitakiwa kufika jana katika kikao kuhojiwa, lakini alikataa.
Katani alisema hiyo ndiyo adhabu ya mwisho kwa Profesa Lipumba,
ambaye hivi karibuni Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis
Mutungi alisema kwa mujibu wa katiba ya chama hicho, bado Lipumba
alikuwa mwenyekiti halali wa chama hicho.
Alisema kutolewa katika vikao halali vya baraza kuu la uongozi ambalo
ndilo lenye uwezo kwa mujibu wa katiba kuwafukuza viongozi wa ngazi za
juu akiwemo mwenyekiti, makamu mwenyekiti na katibu mkuu.
Awali katika kikao hicho, Baraza hilo lilipinga vitendo vya matamshi
ya msajili wa vyama vya siasa, Jaji Mutungi vya kuingilia mambo ya ndani
ya chama hicho ambayo yanakwenda kinyume na kazi yake. Kikao cha Baraza
Kuu la Uongozi wa CUF kilifanyika chini ya mwenyekiti, Katibu Mkuu wa
CUF, Seif Sharif Hamad.
Wakati hayo yakijiri Visiwani, kwa upande wa Bara, Polisi Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam inawashikilia watuhumiwa 22 wanaodaiwa ni
wafuasi wa CUF kwa tuhuma za kupatikana na silaha za jadi za kufanyia
uhalifu, sambamba na kutaka kuchoma moto makao makuu ya ofisi ya chama
hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kamanda wa
Kanda hiyo, Simon Sirro alisema Septemba 25 mwaka huu huko Mwananyamala,
polisi iliwakamata watuhumiwa hao wakiwa na zana za kufanyia uhalifu
yakiwemo mapanga na majambia. “Watuhumiwa hawa pia walikamatwa wakiwa na visu vitano pamoja na
chupa 10 za kupulizia (spray) zikiwa kwenye boksi zenye maandishi ya
Kichina. Watuhumiwa hao walipanda gari la abiria aina ya Coaster yenye
namba za usajili T 857 CHE inayopita njia ya Buguruni- Mwananyamala,”
alisema. Alisema watuhumiwa hao ambao wanashikiliwa kwa mahojiano, walikamatwa
baada ya askari kupata taarifa kwamba wamekuja jijini Dar es Salaam kwa
ajili ya kufanya fujo kwenye ofisi hiyo pamoja na kuichoma moto. “Watuhumiwa hao walipohojiwa zaidi walieleza kuwa wao ni wanachama wa
CUF kutoka Unguja kwenye matawi mbalimbali na wamekuja kwa ajili ya
kazi maalumu na wapo katika kitengo cha ulinzi na kueleza kua wapo zaidi
ya watu 100,” alisema. Alisema, “Katika mahojiano zaidi walieleza kuwa wamekuja jijini Dar
es Salaam kwa maelekezo ya kiongozi wao wa CUF, Nassoro Mazrui ambaye ni
Naibu Katibu Mkuu wa CUF ambaye aliwaamuru kuungana na walinzi wenzao
wengine waliopo ofisi za chama hicho katika makao yao makuu ya CUF
Buguruni”.
Sirro aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Saidi Mohamed Zaharani
aliyekamatwa na boksi la ‘spray’, Hamis Hamisi, Mohisini Ally na Masoud
Igasa Fumu ambao walikamatwa na visu, Juma Omary, Mbaruku Hamisi, Juma
Haji Mwanga, Hamisi Nassoro Hemedi, Mohamedi Omary Mohamed, Nassoro
Mohamed Ally na wenzao 12.
Chapisha Maoni