SERIKALI imeahidi kuboresha na kuimarisha maslahi
kwa watumishi wote wa umma kupitia Bodi ya Mishahara na motisha mara
watakapokamilisha uhakiki wa taarifa za kiutumishi kwa wafanyakazi wa umma,
ambao utawezesha kupanga upya mishahara na motisha kwa watumishi.
Aidha, imesema italipa madeni yote inayodaiwa na
watumishi wake wote mara itakapomaliza kufanya uhakiki huo ili kubaini
watumishi hewa.
Ahadi hiyo ilitolewa jana na Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 55 ya Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam (Udsm).
Katika hotuba yake, Majaliwa alisema Serikali ya
Awamu ya Tano imedhamiria kuhakikisha inaondoa malimbikizo ya madai kwa
watumishi wote wa umma, na mojawapo ya mikakati hiyo ni uhakiki, ambao
unaendelea wa watumishi wa umma. Alisema hadi Oktoba 20, mwaka huu watumishi
hewa, ambao wamebainika kutokana na uhakiki huo walikuwa ni 16,500.
“Baada ya uhakiki huo tutarudia uhakiki wa madeni
yote yaliyowasilishwa serikalini na kisha tutalipa madeni ya watumishi wote
yakiwemo madeni yanayodaiwa na wanataaluma,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Kwa muda mrefu sasa, serikali inaendesha uhakiki
wa watumishi wa umma baada ya kubainika kuwapo na watumishi hewa wengi
wanaolipwa fedha nyingi kila mwezi, hivyo kuipotezea mapato serikali ambayo
yangetumika kwa kazi nyingine, zikiwamo za kuboresha mishahara ya watumishi na
huduma za kijamii.
Akizungumzia changamoto zinazokikabili Chuo Kikuu
cha Dar es Salam likiwemo suala la uhaba wa wahadhiri waandamizi pamoja na
tatizo la mikopo kwa wanafunzi, Majaliwa alisema serikali itaendelea kuweka
kipaumbele cha upatikanaji wa fedha za kutosha kwa ajili ya mafunzo.
Lakini, pia amevitaka vyuo vya umma, kuhakikisha
taratibu na mipango endelevu ya kurithishana kwani bila kufanya hivyo wakati
wote kutakuwa na mapungufu katika utoaji wa taaluma. Alisema serikali
itaendelea kuwaajiri wanataaluma na watumishi wengine wapya pale
wanapohitajika.
Alitoa ahadi hiyo baada ya kuelezwa na Makamu
Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala kuwa chuo hicho kwa sasa
kinakabiliwa na uhaba mkubwa wa wahadhiri waandamizi kutokana na wengi wao
kustaafu.
Kuhusu changamoto ya mikopo ya wanafunzi wa elimu
ya juu, Majaliwa alisema Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya
Ufundi inaendelea kufanya uhakiki wa taarifa za waombaji wa mikopo na akasema
kufikia kesho asilimia 90 ya waombaji ambao wametimiza masharti watakuwa
wameshalipwa fedha zao.
Aliwataka watumishi wa Bodi ya Mikopo ya
Wanafunzi wa Elimu ya Juu kutimiza wajibu wao kuhakikisha kwamba, kwa wale
ambao uhakiki wao umekamilika wapatiwe mikopo hiyo kwa wakati. Alisema kamwe
serikali haitawavumilia watumishi ambao watachelewesha kwa makusudi mikopo ya
wanafunzi wa elimu ya juu.
“Kama kuna taarifa itolewe ndani ya serikali
haraka ili ifanyiwe kazi kuzuia mgogoro kati ya wanafunzi na serikali yao,”
alisema Majaliwa.
Awali, Profesa Mukanda alisema changamoto kubwa
inayokikabili chuo hicho kwa sasa ni uhaba wa wanataaluma waandamizi katika
fani mbalimbali tatizo ambalo alisema linatokana na serikali kusitisha ajira
kwa miaka 10 na hivyo kutoajiriwa wanataaluma chipukizi.
Alisema hali ilivyo kwa sasa katika vyuo vya umma
nchini ni mamia ya wanataaluma wazoefu kustaafu kwa wakati mmoja na wanataaluma
walioajiriwa katika miaka ya hivi karibuni, bado wako masomoni au wangali
chipukizi katika taaluma zao na hivyo kutokuwa na uwezo wa kutosha kubeba
majukumu ya kufundisha shahada za umahiri na uzamivu.
Alisema licha ya serikali kuruhusu utoaji wa
ajira za mikataba kwa wanataaluma wanaostaafu, lakini bado idara nyingi
zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa wanataaluma waandamizi.
Alisema hali hiyo inatishia kukwamisha
utekelezaji wa azma na mpango mkakati wa chuo hicho ambao ni kupanua programu
za mafunzo ya digrii katika ngazi za umahiri na uzamivu.
Kwa hali hiyo aliiomba serikali kutoa mwongozo
utakaosaidia vyuo vikuu vya umma vinavyokabiliwa na changamoto hiyo ili viweze
kuepuka hatari iliyopo ya kushuka kwa viwango ya utoaji maarifa.
“Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kiko tayari kutoa
mchango wa mawazo kuhusu namna ya kuruka kizingiti hicho,” alieleza.
CHANZO: HABARI LEO
Chapisha Maoni