NYOTA wa Filamu na mshindi wa tuzo nyingi za uigizaji nchini Ghana John Dumelo yupo nchini Tanzania akiandaa filamu ya 'Mulasi The Death' katika maeneo mawili ya utalii ya Ngorongoro na Serengeti mtandao wa tanzaniatimes.net umeripoti.
Dumelo yupo na timu inayoongozwa na mtanzania aishiye Marekani Honeymoon Aljabri ambaye pia ni mtunzi, mtayarishaji na muongozaji wa filamu aliyeshinda tuzo kadhaa nchini Marekani.
Dumelo ameeleza, licha ya kuwa na shughuli kubwa ya kurekodi filamu amevutiwa zaidi mandhari na uzuri wa mbuga za wanyama pamoja na huduma bora zinazotolewa katika vivutio vya Serengeti na Ngorongoro.
"Hii ni mara yangu ya pili kufika Tanzania, lakini nchi hii haishi kunishangaza, lazima nirudi kwa ziara ndefu ya utalii," amesema Dumelo ambaye ameshiriki kwenye filamu zipatazo 60 zikiwemo za A Northern Affair, Private Storm, na Tales of Nazir.
John Dumelo ameshinda tuzo ya nyingi ikiwa pamoja na tuzo ya muigizaji bora Afrika, Tuzo za Filamu na muziki za Afro Australia pamoja na tuzo ya muigizaji bora Afrika Magharibi.
Aidha filamu hiyo inayorekodiwa nchini Tanzania inayokwenda kwa jina la 'Mulasi the Death' inategemewa kuzinduliwa mapema mwaka ujao.
Filamu hiyo inayoongozwa na mtanzania Honeymoon Aljabri ambaye pia ni mtunzi, muigizaji na mshindi wa tuzo kadhaa za utayarishaji filamu nchini Marekani amefafanua kuwa 'Mulasi' ni 'Rafiki' kwa lugha ya Kigogo inayopatikana Dodoma, Tanzania na pia inahusisha waigizaji wengine wa hapa nchini.
Chapisha Maoni